Friday, October 3, 2014

WAKAZI JIJINI MBEYA WAHAURIWA KUTUMIA VIZURI FURSA

Mlezi na mshauri wa asasi ndogo
ndogo la kifedha (Vicoba) mkoani
Mbeya, Dk. Stephen Mwakajumilo,
amewataka wananchi wa mkoa huo
kutumia fursa mbalimbali
zinazowazunguka ili kujitegemea
kiuchumi na kuacha kutegemea
wafadhili.
Dk. Mwakajumilo aliyasema hayo
alipokuwa akitoa elimu ya ujasiriamali
kwa waumini wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT) katika mtaa
wa Lwambi, Usharika wa Itete
Halmashauri ya Busokelo wilayani
hapa.
Dk. Mwakajumilo ambaye ni pia
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Teofilo
Kisanji (Teku) cha jijini Mbeya,
alisema wilaya hiyo ni miongoni mwa
wilaya zenye utajiri mkubwa ambao
kama wananchi watautumia vizuri,
watakuwa na fursa nzuri ya kusukuma
gurudumu la maendeleo katika
maeneo yao.
“Nimeelezwa kuna vijana kadhaa
ambao wamemaliza vyuo vikuu kwa
taaluma mbalimbali hapa usharikani,
hakikisheni mnawatumia vijana hao
vyema kwa kuwapeni mbinu za
kufanya katika kutumia vizuri
rasilimali zilizopo ndani ya
halmashauri hii kwa manufaa ya jamii
hii na taifa kwa ujumla,” alisema.
Alieleza kuwa huu siyo muda wa
kuendelea kutegemea wafadhili katika
kuchangia shughuli za kimaendeleo,
wakati wananchi hao wana rasilimali
za misitu na ardhi ambayo ina rutuba
ya kutosha kwa kilimo cha mazao na
nyingine nyingi, hivyo kinachohitajika
ni elimu tu na kukubali kujitoa
kutumia fursa hizo.
“Mfano mzuri ni misitu tuliyonao hapa
kwetu tukiamua kwa dhati
kutengeneza mizinga ya nyuki kadhaa
katika usharika huu, nina hakika
tutaondokana kabisa na suala la
harambee za kila mara kuita watu
kutuchangia kwani tutapata fedha
nyingi ndani ya muda mfupi na
kutimiza malengo yetu,” alisema Dk
Mwakajumilo.
Aidha, alitoa mizinga mitatu na fedha
taslim Shilingi milioni moja kwa ajili
ya kuchonga mizinga mingine ili
kuwahamasisha waumini hao kuanza
rasmi shughuli ya ufugaji wa nyuki
huku akiahidi kupeleka mtaalam wa
nyuki kutoa elimu juu ya utunzaji na
uvunaji bora wa asali.

No comments:

Post a Comment