Thursday, September 25, 2014

CHADEMA NA POLISI WAENDELEA KUZOZANA

Jeshi la Polisi limeendelea
kusuguana na Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema) wakati
wafuasi wa chama hicho wakitaka
kuandamana huku polisi
wakiwadhibiti.
Mkoani Kagera, Jeshi la Polisi
limepanga askari wake kila mtaa
katika manispaa ya Bukoba kwa lengo
la kudhibiti maandamano hayo.
Kaimu Kamanda wa polisi mkoani
Kagera, Gilles Muroto, alisema
kupangwa kwa askari hao
kumetokana na kutoeleweka
maandamano ya wafuasi wa chama
hicho yataanzia katika mtaa upi.
“Tunafahamu siku ya kwanza tutapata
changamoto kutokana na askari
wengi kupangwa kudhibiti
maandamano hayo, lakini kadri
tunavyoendelea tutajipanga vizuri
hakuna shughuli ya kuhudumia
wananchi itakayokwama,” alisema
Muroto.
Alisema kuwa Septemba 22 mwaka
huu walipokea barua ya Chadema
wakiomba kuandamana kesho yake
kuanzia saa 3:00 asubuhi, lakini
maombi hayo hayakukubaliwa
kutokana na kupigwa marufuku na
makao makuu ya jeshi hilo.
Jijini Dar es Salaam, jana polisi
walizizingira ofisi za Chadema makao
makuu kudhibiti wafuasi wa chama
hicho wasiandamane.Askari hao
wakiwamo wa Kikosi cha Kutuliza
Ghasia (FFU), walikuwa katika doria
wakiwa kwenye magari mawili aina ya
Land Rover pamoja na silaha za moto.
Hali hiyo iliwafanya wafuasi wa
Chadema kukaa katika vikundi
wakijadili hali ilivyo katika maeneo ya
kuingilia katika makao makuu ya
chama hicho.Afisa Habari wa
Chadema, Tumaini Makene alisema
wanalishukuru jeshi hilo kwa
kuwasaidia kuandamana katika
maeneo mbalimbali ya nchi.
Aliongeza kuwa wana njia 198 za
kuandamana ikiwa ni pamoja na
kuwatumia ujumbe mfupi viongozi wa
Bunge Maalumu la Katiba kuwaeleza
kuwa hatufurahishwi na
kinachoendelea bungeni.
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, Suleman Kova, alisema
wamejipanga kudhibiti fujo
zitakazotokea. Jijini Mwanza,
Mwenyekiti wa Chadema wa mkoa wa
mwanza, Adrian Tizeba, jana alitiwa
mbaroni na Polisi, baada ya kufanya
mkutano wa waandishi wa habari
kuzungumzia maandamano.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo,
Valentino Kilowoko, alithibitisha
kukamatwa kwa Tizeba na kusema
walikuwa wanaendelea kumhoji.
Kabla ya kukamatwa, Tizeba alilitaka
Jeshi la Polisi mkoani humo
kushirikiana nao katika maandamano
ya amani yatakayofanyika leo kupinga
Bunge la Katiba linaloendelea mjini
Dodoma.
Alisema licha ya polisi wilaya zote za
mkoa wa Mwanza kukataa barua za
taarifa za kuwapo maandamano hayo,
lakini wamekusudia kuandamana na
kuwaomba polisi nao washiriki.
“Haya ni maandamano ya amani,
tunaomba hata polisi washiriki nasi
kesho (leo) ili kufikisha ujumbe wa
matumizi mabaya ya pesa za umma
katika bunge hilo linaloendelea
Dodoma hivi sasa,” alisema Tizeba.

No comments:

Post a Comment