Wednesday, September 24, 2014

KIONGERA KUIKOSA YANGA

Mshambuliaji Paul Kiongera wa
Simba huenda akaikosa mechi ya
kwanza dhidi ya watani wao wa jadi,
Yanga msimu huu wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara itakayopigwa
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam Oktoba 12 baada ya kuumia
goti katika mechi iliyopita.
Kiongera alitokea benchi dakika ya 67
akichukua nafasi ya mfungaji bora wa
msimu uliopita, Mrundi Amissi
Tambwe, lakini dakika mbili kabla ya
mechi hiyo waliyotoka 2-2 dhidi ya
Coastal Union kumalizika, Mkenya
huyo alilazimika kumpisha Amri
Kiemba baada ya kugongana na kipa
Shaaban Kado wa Coastal na kuumia.
Taarifa zilizolifikia NIPASHE jana
kutoka ndani ya uongozi wa Simba
zilieleza kuwa Kiongera ameumia goti
na jana alipelekwa Hospitali ya Taifa
Muhimbili kufanyiwa vipimo.
Mmoja wa viongozi wa Simba (jina
tunalo) alisema mchezaji huyo ana
maumivu sugu ya goti hilo baada ya
kuumia awali akiwa kwao, Kenya.
Kiongozi huyo alisema Kiongera
anaweza kuwa nje ya uwanja kwa
muda wa kati ya wiki sita hadi miezi
miwili kabla ya kuanza mazoezi
mepesi, hivyo hatacheza mechi ya
Oktoba 12 ya watani wa jadi Simba na
Yanga.
Alibainisha kuwa kumeibuka hali ya
wasiwasi ndani ya Simba kwamba
huenda hawakufanya uamuzi sahihi
kumsajili Mkenya huyo kabla ya
kumfanyia vipimo vya afya.
Majeruhi wengine wa Simba ni beki
wa kushoto Issa Rashid ‘Baba Ubaya’
aliyeumia nyama za paja wiki mbili
zilizopita mazoezini, ambaye
inaelezwa kuwa yuko katika wiki ya
mwisho ya mapumziko na winga
Haruna Chanongo aliyeumia goti pia
Jumapili wakati wakichuana na
Coastal. Imeelezewa kuwa Chanongo
atakuwa nje kwa siku nne tangu
kuumia kwake.
Habari njema zaidi kwa Simba kwa
sasa ni kurejea kwa kiungo
mpambanaji Jonas Mkude, ambaye
Daktari wa Simba, Yassin Gembe
amesema anaweza kuanza kucheza
hata Jumamosi dhidi ya Polisi
Morogoro endapo kocha atampanga.
“Ni uamuzi wa kocha tu, lakini ukweli
ni kwamba Mkude yuko fiti kabisa
kwa sasa na anaweza kuanza
kucheza, uzuri ni kwamba pamoja na
kuwa nje kwa muda mrefu, lakini
hajaongezeka uzito,” alisema Gembe.
Mkude hajawahi kuichezea Simba
chini ya kocha aliyerejea kwa mara ya
tatu nchini kuinoa timu hiyo,
Mzambia Patrick Phiri. Katika mechi
iliyopita kiungo Mrwanda Pierre
Kwizera alicheza nafasi ya Mkude
lakini alionekana wazi kutoimudu.
Baada ya Chanongo kuumia, winga
Uhuru Seleman aliingizwa lakini
baada ya mechi kumalizika huku
Coastal wakirudisha mabao yote,
Phiri aliweka wazi kwamba pengo la
Chanongo halikuzibika ipasavyo.
Kikosi cha Simba kilirejea tena
kambini visiwani Zanzibar kujiandaa
kwa mechi yao inayofuata Jumamosi
dhidi ya Polisi Morogoro.

No comments:

Post a Comment