Wednesday, September 24, 2014

KERO YA UMEME MWISHO 2015

Shirika la Umeme nchini (Tanesco),
limesema hadi kufikia Agosti, mwaka
2015, Tanzania haitakuwa na kero ya
shida ya umeme kutokana na
mabadiliko makubwa yanayofanywa
na shirika hilo ikiwamo kuongeza
mitambo ya uzalishaji umeme.
Aidha, shirika hilo limesema
limejipanga kumaliza tatizo la umeme
kutokana na mradi wa kuzalisha
umeme kwa gesi, makaa ya mawe na
kuimarika upatikanaji maji.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi
Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi
Mramba, wakati akikagua miradi ya
ujenzi wa vituo vya Mbagala, Gongo
la Mboto na Kinyerezi 1, jijini Dar es
Salaam inayotarajia kukamilika kati ya
Juni na Agosti, mwaka 2015.
Alisema wakazi wanaozunguka eneo
la Mbagala matumizi yao ya umeme ni
Megawati (MW) 70 na kwamba kituo
hicho kitakapokamilika kitakuwa na
uwezo wa kuzalisha MW 100 kwa
gharama ya Dola milioni 35 za
Marekani.
Kwa mujibu wa Mramba, jijini la Dar
es Salaam pekee linatumia MW 600
kati ya 920 zinazozalishwa kwa sasa
ikifuatiwa na jiji la Arusha, Mwanza,
Tanga na mikoa mingine.
Meneja Mradi Usambazaji Tanesco,
Emmanuel Manirabona, alisema kituo
cha Gongo la Mboto kitakachokuwa
na uwezo wa kutoa MW 50 kinatarajia
kukamilika Desemba mwaka huu.
Akizungumzia kituo uzalishaji umeme
wa gesi Kinyerezi 1, kitakachozalisha
MW 150 alisema miradi hiyo yote
itakapokamilika kero ya umeme nchini
itakwisha.

No comments:

Post a Comment