Tuesday, September 16, 2014

YANGA NI SHIDA TUPU

Baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-0 katika mechi ya Ngao ya Jamii juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Kocha Msaidizi wa Azam, Kally Ongala, amefunguka na kueleza kuwa timu yao ilizidiwa kiufundi katika mechi hiyo.

Akizungumza na NIPASHE mara baada ya mechi hiyo, Ongala alisema makosa yaliyojitokeza watayarekebisha kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi ambapo wao wataanza kampeni ya kutetea ubingwa wao dhidi ya Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Azam Complex.

"Ni bora kufungwa leo kuliko kufungwa kesho, hii itatusaidia kurekebisha makosa kabla ya kuanza kwa ligi, kwa kweli walituzidi kiufundi," alisema Kally ambaye marehemu baba yake alikuwa mwanamuziki maarufu nchini.

Aliongeza kuwa, kupoteza kwa mechi hiyo haiashirii kikosi chao kitaanza vibaya msimu wa ligi.

Katika mechi hiyo Azam ilimkosa nahodha na mshambuliaji wake mahiri, John Bocco, ambaye alikuwa majeruhi.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Yanga Mbrazil Marcio Maximo, yeye alitamba kuwa kikosi chake kina nafasi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara kutokana na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake katika mchezo huo.

Hata hivyo, Maximo alisema licha ya mshambuliaji mpya wa timu hiyo kutoka Brazil, Genilson Santana 'Jaja', kufunga mabao mawili ya kwanza, bado mchezaji huyo anahitaji muda zaidi kujifunza soka la Tanzania. 

Maximo alisema amefurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake hasa katika kipindi cha pili ambacho kilizaa mabao yote matatu.

Alisema anaamini kwa kiwango hicho, Yanga itaweza kurejesha ubingwa ambao ilipokonywa msimu uliopita na Azam ya jijini Dar es Salaam na timu hiyo iliyokuwa chini ya Mholanzi, Hans van Pluijm na msaidizi wake, Boniface Mkwasa. 

Kocha huyo alisema kikosi chake kinajipanga kukabiliana na ushindani na changamoto mbalimbali kutoka kwa timu zote zinazoshiriki ligi hiyo ya Bara yenye timu 14.

"Nina furaha sana leo (juzi), tumeshinda na hii inamaana kwamba kikosi kiko tayari kuanza kusaka ubingwa wa ligi, tumefunga kurasa ya kuufikiria mchezo wa Ngao ya Jamii, tunawaomba mashabiki wa Yanga waendelee kutuunga pia katika mechi za ligi zinazotarajiwa kuchezwa Morogoro, Kagera na Mtwara," alisema Maximo.

Alisema Jaja na mshambuliaji mwingine wa timu hiyo, Andrey Coutinho, wanahitaji muda wa kujifunza vitu mbalimbali vya hapa nchini vya kiufundi, chakula na mazingira kama ambavyo wachezaji Watanzania wanavyokwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

"Sasa akili yetu ni kuanza kampeni mpya ya kujiandaa na mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, tunaanza mazoezi rasmi Jumanne (leo) kwa ajili ya mchezo huo ambao utakuwa ni mgumu kutokana na wachezaji pamoja na kocha wao (Mecky Maxime) wananijua na kuufahamu mfumo wangu," alisema Maximo.
 

No comments:

Post a Comment