Tuesday, September 30, 2014

WAKAZI WA DAR WAPINGA MWEKEZAJI KUZIBA BARABARA

Wakazi wa eneo la Salasala wilayani
Kinondoni, Dar es Salaam wamepinga
uamuzi wa serikali kumpatia kibali
mwekezaji wa kampuni ya Mayfair na
kuziba barabara iliyokuwa ikitumika
kwa miongo miwili.
Mwenyekiti wa Kamati ya usimamizi
wa barabara hiyo, Seleman Magingi,
alisema hatua hiyo ya serikali
itawasababishi usumbufu wakazi
zaidi ya kaya 150 na viwanda.
Alisema mazingira ambayo kibali
hicho kimetolewa, yanaonyesha
viongozi wa Serikali ya Mtaa
kushawishiwa na rushwa.
“Kama mazingira hayo hayakuwa
rafiki mbona wananchi na wenye
viwanda hatukushirikishwa,ndiyo
maana mwekezaji huyo amepata
kiburi,” alisema Magingi.
Mmoja wa wakazi hao,Irene Shayo
alisema viongozi hao wanapaswa
kuangaliwa vizuri kupitia mwekezaji
huyo na kupoteza haki ya wananchi
kwa kununuliwa.
Alisema awali mwekezaji huyo
aliwarubuni kuwa atawaboreshea
miundombinu kama barabara,umeme
na maji wakati huduma hizo
zinapatikana kwa msaada wa viwanda
vilivyopo.
“Kufungwa kwa barabara hiyo
kutasitisha huduma zote za kijamii na
kiuchumi,”alisema.
Afisa Mtendaji wa Mtaa wa
Salasala,Ramadhan Ntai,eneo hilo
limefungwa baada ya mmiliki wa
kiwanja hichi kupata kibali kutoka
Wizara ya Ardhi,Nyumba na Makazi.
Alisema Wizara hiyo ilimtaka
Mwekezaji huyo kufanya marekebisho
ya ujenzi wa kubadilisha matumizi ya
kiwanja hicho ili barabara ipatikane.
Naye, Mmiliki wa Kampuni ya Mayfair
ambaye hakupenda jina lake
liandikwe alisema hayupo tayari
kuzungumza na vyombo vya habari.
“Siwezi kuongea na
waandishi,mtendaji anafahamu kila
kitu mtafuteni yeye,”alisema.
Diwani wa Kata ya Wazo, John Morro,
kupitia barua yake ya Oktoba mwaka
2013 yenye kumbukumbu namba
DSM/KN/2013/22, kwenda kwa
Mkurugenzi wa Ramani wa Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi ikiwataarifu kufufuliwa kwa
barabara hiyo.
Barua hiyo ilikitaka kiwanja namba
10/211 Becon YP 366, 362, 849, 847,
kuacha eneo la barabara kwa ajili ya
jamii.

No comments:

Post a Comment