Uamuzi wa baadhi ya wajumbe wa
Bunge Maalum la Katiba kupiga kura
ya hapana kwa ibara zote za rasimu
mpya ya katiba inayopendekezwa
imeibua mkanganyiko na sasa Kamati
ya Mashauriano imeundwa kukutana
na waliopiga kura hizo.
Juzi wajumbe walianza kupiga kura
kupitisha sura na ibara moja baada ya
nyingine, kwa wazi au siri, huku
wengi wakisema kuwa wanaunga
mkono, lakini pia wakiwamo
wachache waliosema hapana kwa
sura zote 10 na ibara zote kuanzia ya
kwanza hadi ya 157.
Jana Mwenyekiti wa Bunge hilo,
alitaja kamati hiyo kuwa inaundwa na
Makamu Mwenyekiti wa BMK, Samiah
Hassan Suluhu, Rashid Mtuta, Shamsi
Vuai Nahodha, Omari Yusuph Mzee,
Andrew Chenge, Asha-Rose Migiro,
Dk. Francis Michael, Brigedia Jenerali
Mstaafu Hassan Ngwilizi na
Mohammed Aboud.
Bunge hilo limefikia hatua ya kupiga
kura ambayo ni nyeti zaidi kwani
zitahitajika theluthi mbili kutoka kila
upande wa Jamhuri wa Muungano wa
Tanzania ili kufanikisha upitishwaji
wa rasimu hiyo.
Kulingana na mahudhurio
yaliyokuwako juzi kabla ya kuanza
kwa kazi ya upigaji kura, wajumbe
kutoka Tanzania Bara walikuwa 295,
huku kutoka Zanzibar wakiwa ni 142.
Kulingana na hesabu hizo, zitahitajika
kura 140 kutoka Zanzibar na kura 280
kutoka Tanzania Bara ili kupitisha
ibara hizo.
Kwa mahudhurio ya juzi, Zanzibar
ilikuwa na wajumbe wawili zaidi ya
idadi ya theluthi mbili inayohitajika
huku bara kukiwa na wajumbe 15
zaidi ya theluthi mbili ya kura
zinazohitajika.
Hata hivyo, siyo wajumbe wote
walipiga kura za ndiyo na hata
waliopiga za ndiyo wapo waliokataa
baadhi ya ibara. Walikuwapo
waliokataa huku wengine wakipiga
kura za siri, ambazo haijulikani
waliamua nini.
Hali hii inatafsiriwa kama juhudi za
kusaka theluthi mbili ya kura za
wajumbe kutoka Zanzibar, kwa ajili
yakupitisha Rasimu hiyo.
Mwenyekiti wa Bunge hilo juzi
alisema kwa kuzingatia idadi ya
wabunge waliokuwamo bungeni kwa
wakati huo, upande wa Zanzibar
ulikuwa na wajumbe wawili tu
wanaozidi idadi ya inayotakiwa
kupata theluthi mbili, hivyo
akawaomba wote wapige kura ya
ndiyo ili kutimiza matakwa ya
kisheria.
Hata hivyo, zoezi la kupiga kura
lilipoanza, wabunge saba kutoka
Zanzibar walipiga kura ya wazi ya
hapana, huku wengine zaidi ya 20
wakipiga kura ya siri.
Hali hiyo imelifanya BMK kushtuka
kutokana na kuwapo kwa dalili ya
kukosekana kwa theluthi mbili ya kura
za ndiyo kutoka Zanzibar, hivyo
kuufanya uongozi wa Bunge hilo
kuanza kuhangaika kuweka ‘mambo
sawa’.
Kamati ya mashauriano iliundwa kwa
ajili ya kuwasikiliza wajumbe
waliopiga kura ya hapana dhidi ya
rasimu nzima.
Akizungumza saa 5:50 wakati wa
kipindi cha Matangazo jana,
Mwenyekiti wa BMK, alisema kuwa
uongozi umeshtushwa na uamuzi wa
wajumbe hao kupiga kura ya hapana
kwa rasimu nzima huku wakiwa
wametumia muda mwingi kuijadili
jambo ambalo siyo la kawaida.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo,
ameamua kuunda Kamati ya
Mashauriano kwa ajili ya kuwasikiliza,
huku akidai kuwa wajumbe wawili
kati ya waliopiga kura ya kuipinga
rasimu hiyo waliomba kusikilizwa.
Alisema kuwa kanuni ya 54, kanuni
ndogo ya nne inasema kwamba
‘Mwenyekiti baada ya kushauriana na
Kamati ya Uongozi anaweza kuunda
kamati ya mashauriano pale anapoona
linajitokeza suala linalohitaji
mashauriano’.
“Nina suala mbele yangu linalohitaji
mashauriano kutokana na baadhi ya
wabunge wenzetu ambao jana (juzi)
walipiga kura ya hapana kwa ibara
zote kitu ambacho si cha kawaida
kwa sababu haiwezekani kuwa hivyo,”
alisema Mwenyekiti huyo.
“Tunaomba Kamati hii ifanye kazi leo
(jana) na sisi tutapokea matokeo
baadaye na kuyaleta ndani ya Bunge
hili kwa wakati unaofaa,” alieleza
Mwenyekiti huyo.
Alisema kuwa ingawa wajumbe wawili
kati ya waliokataa Rasimu hiyo juzi
walimuomba kusikilizwa pia milango
ya kamati hiyo itakuwa wazi hata kwa
wajumbe wengine ambao hawajaomba
ili ieleweke kwanini wakae wakati
walikaa kipindi chote bungeni kisha
waikatae rasimu yote.
Baadhi ya wajumbe wa BMK
waliozungumza na NIPASHE jana
mjini Dodoma walielezea
kutoridhishwa na hatua hiyo,
wakiamini kanuni ililenga kuundwa
kwa kamati wakati wa vipindi vingine
vya uhai wa BMK, lakini siyo katika
kipindi hiki cha upigaji kura.
Walisema kuwa kitendo cha kuundwa
kamati hiyo katika kipindi cha kupiga
kura, wanakitafsiri kuwa ni kuingilia
uhuru wao wa kufanya maamuzi.
Dk. Alley Nassoro, alisema yeye siyo
miongoni mwa walioelezwa na
Mwenyekiti wa BMK, kuwa wameomba
kusikilizwa na kwamba hajutii kupiga
kura ya hapana kwa rasimu yote kwa
sababu ana amini ndiyo msimamo
halisi alionao juu ya kazi yote
aliyofanya tangu BMK lilipoanza.
“Sababu zangu kuu ni mbili tu
ambazo zimesababisha nipige kura ya
hapana, ya kwanza ni imani na uzawa
wangu; nikimaanisha dini ya kiislamu
kunyimwa haki ya Mahakama ya Kadhi
kutambuliwa na kuheshimiwa kikatiba
lakini ya pili ni maslahi ya nchi yangu
Zanzibar, kutozingatiwa na Katiba hii
kwa kiwango cha kukidhi matarajio
yangu,” alisema Dk. Alley.
Alisema hata ahadi iliyotolewa
bungeni na Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, wakati wa mijadala ya
kuboresha Rasimu hiyo ya Katiba
inayopendekezwa, kwamba Mahakama
ya Kadhi itatungiwa sheria haafikiani
nayo kwa sababu siyo mara ya
kwanza kwa serikali kutoa ahadi juu
ya jambo hilo.
Alisema kwamba hata ikitungwa
sheria ya aina hiyo, utekelezaji wake
unaweza usifanyike kwa sababu
utategemea zaidi uongozi
utakaokuwa madarakani tofauti na
kama haki hiyo ingewekwa kwenye
Katiba ambayo ndiyo sheria mama.
“Hii Katiba inayopendekezwa kwa
jinsi ilivyowekwa ni dhahiri hata
kama ikitungwa sheria ya kuanzisha
Mahakama ya Kadhi, utekelezaji wake
utakuwa mgumu kwa sababu baadhi
ya watu wanachukulia baadhi ya
masharti katika imani yetu kuwa ni
yenye chembe za kibaguzi hususan
katika umiliki wa mali baina ya
mwanamke na mwanaume,” alieleza
Dk. Aley.
Suala la kupata theluthi mbili ya kura
za upande wa Zanzibar linakuwa tete
kutokana na wabunge wa Chama cha
Wananchi, CUF pamoja na wale wa
kundi la 201 ambao waliungana na
kundi la Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) na kuondoka
bungeni, hali inayosababisha idadi ya
wajumbe waliobaki kupata wakati
mugumu kutimiza matakwa ya
kisheria ya kuhakikisha Rasimu hiyo
inapitishwa na theluthi mbili ya kura
za wajumbe wote kutoka katika kila
nchi washirika.
Imeandaliwa na Emmanuel Lengwa,
Editha Majura, John Ngunge na
Jacqueline Massano, Dodoma.
Saturday, October 4, 2014
BUNGE LA KATIBA MSHTUKO
Labels:
habari
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment