Wednesday, October 8, 2014

MAANDALIZI YA KUKABIDHI KATIKA MPYA KWA KIKWETE YAKAMILIKA

Wakati Maandalizi ya kuwakabidhi
Rais Jakaya Kikwete na Rais wa
Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein
Katiba inayopendekezwa, leo mjini
Dodoma, vyama vinavyounda Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
vimesema havitashiriki tukio hilo kwa
madai kuwa maoni ya wananchi
yamechakachuliwa.
Vyama hivyo ni Chadema, CUF na
NCCR-Mageuzi.Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk. Willibrod Slaa
(pichani), alisema wao hawatashiriki
kwa madai ya kwamba mawazo ya
wananchi yaliyokuwamo kwenye
Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na
iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, yalichakachuliwa.
“Sisi Chadema hatutashiriki kwa
sababu mawazo ya wananchi
yamechakachuliwa. Makundi
mbalimbali kama vile ya wakulima,
wafugaji yamekuwa yakichukuliwa
kwa makundi na kuambiwa
wakubaliane na katiba
iliyopendekezwa. Wananchi hao
hawana uelewa wa kutosha, hivyo
wanaamini kiongozi wao
anachokisema hata kama ni uongo.
Tunafanya usanii, sisi Chadema
hatuko tayari kushiriki usanii huo.”
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James
Mbatia, alisema hawezi kusema
chochote kuhusu makabidhiano hayo,
kwa kuwa hawajapewa mwaliko
wowote.
Kwa mujibu wa Mbatia, ofisi yake
ingepewa mwaliko wa kuhudhuria
tukio hilo, angeweza kujua kitu gani
kilichomo kwenye barua na hivyo
kuweza kusema chochote kuhusu
tukio hilo linalotarajia kufanyika leo
katika Uwanja wa Jamhuri, mjini
Dodoma.
“Hatujaalikwa. Mimi kama mwenyekiti
wa chama, ningepata mwaliko,
ningeona maudhui na kujua la
kusema. Sasa nitawezaje kusema,
ikiwa hatujaalikwa na maudhui
siyajui?” Alihoji Mbatia.
Hata hivyo, alisema, wao hawawezi
kujihusisha kwenye tukio ambalo
halina maridhiano kwa madai ya
kwamba, dola inaendeshwa kwa
maridhiano huku akionyesha
kusikitishwa na hatua iliyofikiwa na
BMK ya kuwatukana viongozi wa dini
wakati zoezi la mwisho la kuipigia
kura katiba hiyo iliyopendekezwa na
bunge hilo wiki iliyopita.
“Nchi bado haijakaa vizuri, nami
siwezi kushiriki kupokea katiba
inayounganisha nchi ya namna hiyo.
Hivyo namshauri Rais, leo
azungumze namna ya kuliunganisha
taifa.”
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF,
Joran Bashange, alisema, wao
walishakataa baada ya kuona
mchakato wa upatikanaji wa katiba
mpya ulikuwa unaenda kinyume na
matakwa ya wananchi.
“Wamepanga utaratibu wao, sisi
tutakubalianaje? Sisi tulikataa kwa
sababu tuliona mchakato ulikuwa
unaenda kinyume cha matakwa ya
wananchi. Hivyo hatuwezi kwenda
kubariki uharamia.”
Naye mjumbe wa iliyokuwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba (TMK), Prof.
Mwesiga Baregu, alishauri tukio la
kukabidhi katiba inayopendekezwa,
lifanyike kimya kimya.
“Ninasikia kuwa kuna maandalizi ya
sherehe za kukabidhi Katiba hiyo
yanayoambatana na nyimbo mpya
zilizoandaliwa kwa ajili ya kuimbwa
kwenye tukio...mimi nashauri
makabidhiano yafanyike kimya
kimya,” alisema Prof. Baregu na
kuongeza:
“Ninashauri hivyo kwa sababu kwa
sasa inaonekana kwamba hatua ya
kupitisha katiba hiyo imekuwa kama
ni ushindi kwa wale walioipitisha na
kumbe sivyo.”
“Watanzania wanataka Katiba
inayowaunganisha na siyo
inayowatengenisha, hivyo kuruhusu
sherehe kwenye makabidhiano hayo
ni kuendeleza msuguano miongoni
mwa makundi yanayopingana kuhusu
katiba hiyo," alisema.
Prof. Baregu alisema kuwa cha msingi
ambacho kilikuwa kinatakiwa ni
maridhiano ili kupata kile wananchi
wanakihitaji, hivyo kushangilia ama
kusherehekea bila kuwa na
maridhiano ni kuongeza mpasuko
kwenye jamii.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk.
Rehema Nchimbi, alisema hadi jana
mchana, tayari mazingira ya uwanja
wa Jamhuri yalikuwa tayari
yameshaandaliwa.
Hata hivyo alipoombwa kutaja majina
ya viongozi wakuu waliothibitisha
kuhudhuria sherehe hizo, Dk. Nchimbi
alisema orodha ipo kwa Katibu wa
BMK kwani wao ndiyo wanaoratibu
shughuli hiyo.
Kwa mujibu wa tarifa za awali
zilizopatikana kutoka kwa ofisa
mmoja wa serikali, sherehe hizo
zinatarajiwa kuhuduriwa na wageni
takribani 3,000.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa,
David Misime, alisema
wamejiimarisha kiulinzi na kwamba
kutakuwa na doria katika maeneo
mbalimbali yakiwamo ya mjini.
“Tunafuatilia taarifa mbalimbali kwa
ajili ya kuimarisha usalama, vijana wa
kufanya doria kwa miguu, farasi,
pikipiki na magari wapo muda wote
kuanzia sasa,” alisema Kamishna
Misime.

No comments:

Post a Comment