Saturday, October 4, 2014

KLA

Klabu za ligi kuu ya Bara zinakusudia
kupeleka katika mkutano mkuu wa
shirikisho la soka (TFF), hoja ya
kutokuwa na imani na rais Jamal
Malinzi.
Klabu hizo, kupitia kwa wakili Dk.
Damas Ndumbaro, zilisema jijini jana
kwamba zitakusanya theluthi mbili ya
kura za wanachama wa TFF ili
kuitisha mkutano mkuu na kupeleka
hoja mbili, ikiwemo hiyo ya
pendekezo la kumng'oa rais
madarakani.
Mkutano mkuu wa TFF una madaraka
ya kumuondoa rais madarakani
kikatiba.
Mbali na hoja ya kutokuwa na imani
na Malinzi, pia klabu zitawasilisha
hoja ya kutaka kufanyike ukaguzi wa
hesabu za fedha za TFF zinazotolewa
na wadhamini wa ligi kuu tangu
kuingia madarakani kwa Malinzi,
Ndumbaro alisema.
Hatua hizo zinafuata baada ya klabu
hizo kuiagiza Bodi ya Ligi Kuu (TPLB)
kutokubali makato ya ziada ya
asilimia tano ya fedha za wadhamini.
TFF imedai inataka kupeleka fedha
hizo kwenye mfuko wa TFF wa
maendeleo ya soka ya vijana.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini jana, Ndumbaro alisema klabu
hazikubali makato ambayo TFF
imeagiza.
"TFF inapata fedha nyingi zaidi ya
vilabu kwa mwaka," alisema
Ndumbaro. "Kwa mfano katika
udhamini wa Azam TFF peke yake
inaingiza zaidi ya milioni 400 huku
vilabu vikiingiza milioni 331.
"Lakini bado katika fedha hizo ndogo
wanazopata vilabu TFF wanataka
kuzikata... kimsingi wateja wangu
(klabu) hawakubali na wanalipinga
suala hili."
Aidha, Ndumbaro alisema kukatwa
Sh. 1000 kabla ya kodi katika mapato
ya kila tiketi iliyotumika kuingia
uwanjani ni hujuma inayofanywa na
TFF kwa serikali, klabu na chama cha
mapinduzi kinachomiliki viwanja vingi
vya soka nchini.
Alisema serikali inadhulumiwa kwa
kodi kutolipwa kwa Mamlaka ya
Mapato (TRA) na hivyo kurudisha
nyuma maendeleo ya nchi na ya klabu
za ligi kuu.
Ndumbaro alisema kugomea kucheza
ligi kuu ni moja ya njia ambazo klabu
zimepanga endapo muafaka
hautapatikana.
Ndumbaro alisema klabu zipo tayari
kukutana na TFF kwa muzungumzo.

No comments:

Post a Comment