Wednesday, October 8, 2014

SIMBA YAENDA KAMBI S.AFRICA KWAAJILI YA MAANDALIZI YA MECHI DHIDI YA YANGA

Kikosi cha Wekundu wa Msimbazi
kimebadili muelekeo na sasa
kinatarajia kuondoka nchini leo,
Jumatano kuelekea Afrika Kusini kwa
ajili ya kuweka kambi kujiandaa na
mechi ya mzunguko wa kwanza dhidi
ya watani wao jadi, Yanga
utakaochezwa Oktoba 18, mwaka huu
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam.
Awali NIPASHE ilifahamishwa kwamba
Simba ingekwea pipa kuelekea
Muscat, Oman kwa ajili ya kambi
hiyo, lakini ghafla ikabadili muelekeo
huo.
Kikao cha Wajumbe wa Kamati ya
Mashindano kilichokutana juzi jioni
ndicho kilichofikia maamuzi hayo
baada ya kuwa na mapendekezo
mawili ya kuipeleka timu Oman au
Afrika Kusini kujifua.
Akizungumza na gazeti hili jana,
kiongozi mmoja wa klabu hiyo yenye
makao makuu mtaa wa Msimbazi,
Kariakoo jijini, alisema kuwa timu
hiyo itaweka kambi ya siku 10 katika
jiji la Johanesburg.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo
zinaeleza kuwa awamu ya kwanza ya
wachezaji wataondoka jijini leo jioni
na kundi la pili ambalo litakuwa na
wachezaji walioko katika kikosi cha
timu ya Taifa (Taifa Stars) kitaondoka
Jumapili usiku.
Taarifa zaidi zinaeleza kwamba
huenda timu hiyo ikiwa Afrika Kusini
itacheza mechi moja ya kirafiki ya
kimataifa na klabu mojawapo
inayoshiriki Ligi Kuu ya nchi hiyo na
taratibu za kupata mchezo huo
zimeshaanza.
"Timu itaondoka kesho (leo) jioni na
itarejea siku moja kabla ya mechi,"
alisema kiongozi huyo.
Alisema kuwa wanaamini kambi hiyo
itasaidia kuimarisha kikosi chao na
sare walizopata hazijawakatisha
tamaa.
Simba ina pointi tatu baada ya kupata
sare tatu mfululizo katika mechi zake
zilizotangulia dhidi ya Coastal Union
ya Tanga, Polisi Morogoro na Stand
United kutoka mkoani Shinyanga.
Yanga yenyewe itashuka dimbani
ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa
mabao 2-1 walioupata dhidi ya JKT
Ruvu ya Pwani na Prisons, lakini
wakiwa na doa la kichapo cha 2-0
kutoka kwa Mtibwa Sugar ya
Manungu, mkoani Morogoro katika
mechi ya ufunguzi wa ligi hiyo.
Awali mechi hiyo ya watani wa jadi
ilipangwa kufanyika Oktoba 12 lakini
ikasogezwa mbele na Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) ili kupisha
maandalizi ya timu ya Taifa (Taifa
Stars) kuikabili Benin katika mchezo
wa kirafiki wa kimataifa.

No comments:

Post a Comment