Wednesday, September 24, 2014

JUMLA YA Tshs. BIL. 6 YATENGWA KWAAJILI YA MIKOPO YA VIJANA

Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo, imetenga Sh. bilioni 6.0
kwa mwaka wa fedha 2014/2015 ili
kuwasaidia vijana kupata mikopo.
Mikopo hiyo itawawezesha vijana
kujiajiri wenyewe na kutengeneza
ajira kwa vijana wengine.
Mkurugenzi wa Uwezeshaji wa wizara
hiyo, Dk. Kissui Steven Kissui,
aliyasema hayo jijini Dar es Salaam
jana wakati akizungumza na
waandishi wa habari.
Alifafanua kuwa fedha hizo zitatolewa
kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana
kwa lengo la kuwasaidia kupata
mikopo yenye masharti nafuu ili
kuwajengea uwezo kiuchumi kwa
kuanzisha na kuimarisha miradi yao
na kuwawezesha kujitegemea katika
kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja
na hatimaye nchi nzima.
“Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya
Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007,
kijana ni mtu yeyote mwenye umri
kati ya miaka 15 na 35, hivyo vijana
wote walio katika umri huo ni
walengwa wa mfuko huu,” alifafanua
Dk. Kissui.
Aidha, alisema kutokana na
changamoto zilizojitokeza hususani
katika urejeshaji na usimamizi wa
mikopo inayotolewa, serikali iliamua
kubadili utaratibu wa utoaji mikopo
hiyo na kuunda utaratibu mpya
ambao ulianza kutumika Aprili, 2013.
Alisema mikopo ya mfuko huo
hutolewa kupitia miradi ya vijana
iliyoidhinishwa kwa pamoja kati ya
wizara, mikoa, halmashauri na
hatimaye fedha hizo kupitishwa
saccos za vijana.
“Mwaka 2013/2014, mikopo yenye
thamani ya Shilingi 415,919,000
ilikopeshwa kwa vikundi vya vijana 67
kutoka katika halmashauri 25 za
Tanzania bara na wizara bado
inaendelea kupokea na kuchambua
maandiko ya miradi kutoka katika
halmashauri mbalimbali,” aliongeza.
Aidha, alisema wizara inaendelea
kuwahamasisha vijana kujiunga
katika vikundi vya ujasiriamali ikiwa
ni pamoja na kusajili vikundi hivyo na
hatimaye kujiunga na saccos za
vijana zilizoanzishwa.
Dk. Kissui alisema pia fedha za Mfuko
wa Maendeleo ya Vijana ni kwa ajili
ya vijana wote nchini, hivyo kila
kijana anayo haki ya kunufaika na
mkopo kutoka katika mfuko huo ikiwa
ni pamoja na kukopa na kurejesha.
Hata hivyo, aliwaomba wananchi
kutohusisha fedha hizo na masuala
ya kisiasa wakidhani kuwa ni zawadi.

No comments:

Post a Comment