Tuesday, September 16, 2014

MAKUNDI MATANO YA DANCE 100% YATINGA NUSU FAINALI

Safari ya shindano la Dance 100% imefikia patamu baada ya juzi makundi matano kati ya makundi kumi yaliyochuana vikali katika nusu fainali kwenye uwanja wa Don Bosco Oysterbay jijini Dar es Salaam kutinga fainali.

Shindano hilo linaloandaliwa na kituo cha televisheni cha East Africa (EATV) na kudhaminiwa na Vodacom Tanzania limeleta mapinduzi makubwa katika tasnia ya kudansi nchini na kuwavutia vijana wengi kushiriki.

Makundi ya wachezaji wa miondoko mbalimbali ya muziki yaliyoingia fainali ni Wazawa Crew, Best Boys Crew, The W.T, Wakali Sisi na The Winners Crew.

Mratibu wa mashindano hayo, Happy Shame, alisema kuwa katika kinyang’anyiro cha nusu fainali hiyo wamepata makundi matano yaliyoingia fainali itayofanyika baadaye.

“Huu ni mwaka wa tatu EATV tunaandaa mashindano haya chini ya udhamini wa Vodacom Tanzania. Mwaka huu mashindano haya yamekuwa na umaarufu mkubwa na ushindani wa hali ya juu na kuwavutia vijana wengi ambao hujitokeza kushiriki,”alisema Shame.

Shame aliongeza kuwa kundi litakaloibuka na ushindi katika mashindano haya ambayo pia yamekuwa yakioneshwa na kituo cha EATV kila Jumatano saa moja kamili usiku, litajishindia kitita cha Sh. milioni 5.

Naye Meneja Uhusiano wa Umma wa Vodacom Tanzania ambao ni wadhamini wakuu wa shindano hilo, Matina Nkurlu aliwapongeza vijana wote walioshiriki katika shindano hilo na kuwapa moyo wale ambao hawakufanikiwa kuingia fainali kuwa wasife moyo kwani asiyekubali kushindwa si mshindani bali wajipange upya na wawe wabunifu zaidi na kuweza kushiriki tena mwakani.

No comments:

Post a Comment