Wednesday, September 24, 2014

TIKETI ZA KIELEKTRONIKI ZAANZA KUJIBU

Mfumo wa tiketi za elektroniki katika
mechi za soka nchini umeanza kuzaa
matunda baada ya jana Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), kuweka wazi
kwamba mapato ya milangoni
yameongezeka.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam jana mchana,
Mkurugenzi wa Mashindano wa
shirikisho hilo, Boniface Wambura,
alisema utumiaji wa tiketi za
elektroniki umefanikiwa kudhibiti
hujuma za mapato ya milangoni
kwenye viwanja ambavyo tayari
vimeshasimikwa mfumo huo.
Wambura alisema kwa sasa wanapata
mapato halisi ya mechi husika
kulingana na idadi ya watu waliokata
tiketi.
“Hatutarudi nyuma katika hili,
tutaendelea kutumia tiketi za
elektroniki kwenye viwanja vyote
vilivyosimikwa mfumo huu,” alisema
Wambura na kuongeza: “Kuna viwanja
kama CCM Kirumba jijini Mwanza na
Sheikh Amri Abeid jijini Arusha vina
mfumo huu lakini havitumiwi na timu
za Ligi Kuu.
Tutahakikisha mechi za Ligi Daraja la
Kwanza zinazochezwa kwenye
viwanja hivyo vinatumia tiketi za
elektroniki ili watu waishio katika
majiji hayo pia wauzoee.”
Mkurugenzi huyo alisema watu wote
wanaojaribu kuingia viwanjani kwa
kutumia tiketi feki wamekuwa
wakinaswa kwa kutumia mashine za
utambuzi wa tiketi za elektroniki
(PDA), hivyo kwa sasa hakuna mtu
anayeingia kwenye viwanja vilivyo na
mfumo huo akitumia tiketi bandia.
Akitangaza mapato ya mechi za wiki
iliyopita za Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara (VPL), Wambura
alisema yameongezeka kwa kiasi
kikubwa, sababu kubwa akisema ni
matumizi ya mfumo wa tiketi za
kisasa za kielektroniki.
Wambura alisema mechi ya Mtibwa
Sugar dhidi ya Yanga iliyochezwa
kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini
Morogoro Jumamosi na kumalizika
kwa wenyeji kuibuka na ushindi wa
mabao 2-0, imeingiza Sh. milioni 59
kutokana na viingilio vya mashabiki
11,499 waliokata tiketi za Sh. 5,000.
Mapato hayo ni ongezeko la Sh.
milioni 12 ikilinganishwa na mapato
ya mechi kati ya timu hizo kwenye
uwanja huo msimu uliopita.
Aidha, Wambura alisema kuwa mechi
ya Simba dhidi ya Coastal Union
iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam Jumapili huku
timu hizo zikitoka sare ya mabao
mawili, imeingiza Sh. milioni 124.7
zilizotokana na viingilio vya
mashabiki 22,114 waliokata tiketi
kuingia kwenye uwanja huo wenye
uwezo wa kuketisha watazamaji
57,558.
Simba na Coastal Union ziliingiza Sh.
milioni 36.8 zilipokutana katika mechi
ya ligi hiyo kwenye uwanja huo
msimu uliopita.
Utumiaji wa tiketi hizo za kielektroniki
ni utekelezaji wa mapendekezo
yaliyomo kwenye ripoti ya Kamati
Maalum ya Kudhibiti na Kuboresha
Mapato ya TFF iliyotolewa 2011 na
agizo la serikali lililotolewa katikati
ya mwaka huu.
Mei 2011 Kamati Maalum ya Kudhibiti
na Kuboresha Mapato ya TFF
iliyoongozwa na Rais Mstaafu wa
shirikisho hilo, Leodegar Tenga, ilitoa
ripoti yenye kurasa 95 ikionesha
uhujumu mkubwa wa mapato
utokanao na matumizi ya tiketi za
kawaida, hivyo kamati ikapendekeza
TFF ianze kutumika tiketi za kisasa za
kielektroniki.
Aidha, Juni mwaka huu, serikali
iliiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) kuiiamuru TFF kutumia mfumo
wa tiketi za kielektroniki kwenye
viwanja mbalimbali vya soka nchini ili
kudhibiti uhujumu wa mapato ya
milangoni.
Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya
Bunge ya Uchumi, Viwanda na
Biashara kuhusu utelezaji wa
majukumu ya Wizara ya Fedha na
Uchumi kwa mwaka wa fedha 2014/15
Bungeni mjini Dodoma Juni 4, mwaka
huu, mwenyekiti wa kamati hiyo,
Luhaga Mpina aliitaka TRA kutoa
sharti kwa TFF kutumia mfumo wa
tiketi za elektroniki ili kuongeza
mapato ya nchi.
"Kamati inashauri TRA iweke sharti la
lazima la kuitaka TFF kutumia mfumo
wa tiketi za kielektroniki katika kuuza
tiketi zake ikiwa ni jitihada za
kuongeza mapato ya serikali," alisema
Mpina.
Mbunge huyo wa Kisesa (CCM),
alisema kwa muda mrefu serikali
imekuwa haipati mapato ya kutosha
kutoka katika sekta ya michezo
hususan mpira wa miguu ulio chini ya
TFF kutokana na mfumo dhaifu wa
ukusanyaji fedha kipindi cha kuuza
tiketi.

No comments:

Post a Comment