Monday, September 15, 2014

JE WAJUA KUA FEDHA ZILIZOTUMIKA KATIKA MAANDALIZI YA KATIBA MPYA ZINGEWEZA KUTANDIKWA BARABARA YA KUTOKA DAR MPAKA....

Taifa linaelekea kupata hasara kubwa
ya zaidi ya Sh. bilioni 120 baada ya
kushindwa kupatikana kwa katiba
mpya kama ilivyokusudiwa.
Kiasi hicho cha fedha zitakazopotea
bure kinatokana na makadirio ya
jumla ya fedha zitakazojumuisha
mchakato wote uloiodumu kwa zaidi
ya mwaka mmoja sasa, ukianzia
wakati wa kuundwa kwa Tume
Maalum ya Mabadiliko ya Katiba na
pia kuwapo kwa vikao vya Bunge
Maalum la Katiba vinavyoendeloea
mjini Dodoma na kutarajiwa
kusitishwa Oktoba 4 mwaka huu.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE na
kuwahusisha wachambuzi mbalimbali
wa masuala ya siasa na uchumi
umebaini kuwa kwa kukadiria, ikiwa
wajumbe wote waliopo bungeni hivi
sasa watakuwa wakihudhuria kila
kikao katika ngwe ya pili iliyoanza
Agosti 5, maana yake ni kwamba kila
mmoja ataondoka na Sh. milioni 12.9
za posho za siku 43 za kazi pamoja
na fedha nyingine kiasi cha Sh.
4,140,000 zitakazotokana na posho
watakayoipata katika siku 18
zisizokuwa za kazi.
Inaelezwa kuwa wajumbe hao hulipwa
posho ya Sh. 300,000 kila mmoja
katika siku za kazi wanazohudhuria
kikao huku wanapokosa kikao kwa
ruhusa maalum, pamoja na siku
zisizokuwa za kazi hupokea posho ya
Sh.230,000.
Hadi sasa, wajumbe waliojisajili
baada ya kuanza kwa ngwe ya pili
wanakadiriwa kuwa 528, idadi ambayo
haihusishi wajumbe 101 wakiwamo
wanaotoka katika kundi la Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao
walisusia vikao hivyo tangu April 16,
2014 wakipinga kubadilishwa kwa
rasimu iliyowasilishwa na Tume
iliyoongozwa na Warioba kutokana
maoni yaliyokusanywa kutoka kwa
wananchi.
Inaelezwa kuwa kwa hesabu hizo,
jumla ya kiasi cha fedha
kitakachotumika tangu kuanza tena
kwa Bunge hilo Agosti 5 hadi Oktoba
4 kitapanda zaidi kwani hadi
kusitishwa kwa bunge hilo katika
awamu hii ya pili, kila mmoja
atakayehudhuria bila kukosa atapokea
jumla ya Sh. 17,040,000.
Hadi kufikia mwishoni mwa wiki
iliyopita hakukuwa na takwimu rasmi
kutoka ofisi ya Bunge Maalum la
Katiba kuhusiana na idadi ya
wajumbe waliopo kwenye bunge hilo
linaloendelea mjini Dodoma.
Hata hivyo, inakadiriwa kuwa
wajumbe wa Bunge hilo waliopo nje
ni wabunge 62 kutoka kambi ya
Upinzani bungeni, wajumbe 30 wa
Chama Cha Wananchi (CUF)
wanaotoka katika Baraza la
Wawakilishi huku wajumbe wengine
wakiwa ni pamoja na wafuasi wa
vyama vinavyounda Ukawa vya Chama
cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), NCCR-Mageuzi na pia
CUF, walioingia kupitia kundi la
wajumbe 201 walioteuliwa na Rais
ambao miongoni mwao ni pamoja na
Profesa Ibrahim Lipumba, Profesa
Abdallah Safari, Julius Mtatiro na
Mchungaji Christopher Mtikila wa DP.
Fedha nyingine zilizotumiwa na taifa
kugharimia mchakato huo ni Tume ya
Mabadiliko ya Katiba iliyotumia Sh.
bilioni 67.888 katika kipindi cha
takribani mwaka mmoja wa uhai
wake, ukarabati jengo la Bunge
ukigharimu Sh. bilioni 8.6 na awamu
ya kwanza ya Bunge hilo ikitumia Sh.
bilioni 27 kwa siku 67; hivyo gharama
za jumla kuwa zaidi ya Sh. bilioni 120
TUME YA KATIBA
Iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba ilitumia takribani Sh. bilioni 69
ambazo Waziri Kivuli katika Wizara ya
Katiba na Sheria, Tundu Lissu,
aliwahi kueleza bungeni kuwa ni
kufuru.
Katika bajeti ya mwaka wa fedha
2013/14, Bunge liliidhinisha Sh.
bilioni 33.944, sawa kiasi kile kile
kilichoidhinishwa mwaka wa fedha
uliopita.
Fedha hizo zilitumika kulipa posho
kwa wajumbe na maofisa wengine wa
tume, usafiri, nyumba kwa waliokuwa
wanatoka nje ya Dar es Salaam na
chakula.
Kadhalika, katika fedha hizo, Serikali
pia iliomba Sh. milioni 18 kwa ajili ya
kugharamia chakula kwa Wajumbe wa
Tume na Sekretarieti watakaopata
maambukizi ya ukimwi.
UKARABATI BUNGE
Taarifa zinaeleza kuwa Sh. bilioni 8.6
zilitumika kukarabati ukumbi wa
Bunge ili kuweza kuhudumia wajumbe
629 na miundombinu yake na kuweka
vifaa vya kisasa vikiwamo vya
usalama.
Ukarabati ulihusisha jengo la bunge
na miundombinu yake kwa kuweka
viti vipya 678 vilivyofungwa kwenye
ukumbi huo uliokomba Sh. bilioni 1.6,
kurekebisha mfumo wa sauti uliokuwa
hausikiki vizuri na kuweka baadhiya
vipaza sauti, kuweka vioo
visivyopenyeza risasi, paa na Idara ya
Kuhifadhi Kumbukumbu za Bunge
(hansard).
BUNGE MAALUM
Mei mwaka huu, Waziri wa Fedha,
Saada Mkuya, alikaririwa akisema
Serikali ilitumia Sh. bilioni 27
kuendesha Bunge Maalum la Katiba
kwa siku 67 za awali kabla ya
kusitishwa kupisha Bunge la Bajeti.
Bunge hilo ambalo lilirejea tena
Agosti 5, kwa siku nyingine 60,
inaweza kugharimu zaidi ya Sh.
bilioni 20.Hata hivyo, Serikali inaweza
kuokoa fedha kidogo baada ya
makubaliano kati ya Rais Jakaya
Kikwete na Wanachama wa Kituo cha
Demokrasia (TCD) wakiwamo
wajumbe wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), kuafikiana kuwa
sasa Bunge hilo lisitishwe Oktoba 4
badala ya Oktoba 31; kisha Katiba ya
Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977
itafanyiwa marekebisho ili itumiwe
kwenye uchaguzi mkuu wa mwakani.
Makubaliano hayo yamekuwa pigo
kwa walalahoi nchini ambao
walidhani wangepata Katiba mpya na
badala yake Katiba ya sasa itawekwa
'viraka' .
Mbali ya posho, kuna matumizi
mengine kama mafuta ya magari,
vipuri, karatasi, viburudisho,
mawasiliano, umeme wa viyoyozi,
maji, karatasi za vyoo, machapisho,
kukirimu wageni, kualika wataalamu
kutoa ufafanuzi na safari za kikazi, ni
wazi kuwa mabilioni yameyeyuka.
HASARA KWA TAIFA
Fedha hizo zaidi ya Sh. bilioni 120
zinazoendelea kupotea kwa
kushughulikia katiba ambayo
imethibitika kuwa kwa sasa
haitapatikana kama ilivyotarajiwa, ni
hasara kubwa kwa taifa kwani
zingeweza kutumika katika maeneo
mengi ya maendeleo.
Kwa mfano, inaelezwa kuwa fedha
hizo zingesaidia sana kupunguza
tatizo la foleni za magari jijini Dar es
Salaam kama zingeelekezwa kwenye
mradi wa ujenzi wa barabnara za
pembezoni (ring roads).
Katika bajeti ya mwaka wa fedha wa
2013/2014, Wizara ya Ujenzi ilieleza
kuwa vipaumbele vyake ni pamoja na
kupunguza foleni jijini Dar es Salaam
ikiwa ni pamoja na Ujenzi wa
barabara ya Kigogo – Jangwani (Sh.
bilioni 7.6), fidia kwa majengo ya
kandoni mwa barabara ya Kigogo-
Jangwani (Sh. bilioni 15.8) na
kipande cha kilomita tatu cha
barabara ya Kimara Korogwe-
Kilungule kinachogharimu Sh. bilioni
3.5. Fedha nyingine ni ni Sh. bilioni
13 kwa ajili ya kilomita saba za Mbezi
Mwisho-Goba, Sh. bilioni 16 za Tangi
Bovu-Goba, Baruti-Msewe (Sh.
bilioni 4.6) na Kigogo- Tabata Dampo
(Sh. bilioni 5.7). Miradi hii yote
ingekamilishwa mara moja kwa
mabilion yaliyoelekezwa kwenye
mchakato wa kuandika katiba.
Fedha hizo za kugharimia katiba
zingetosha pia kujenga zahanati za
kisasa 600 ikiwa kila moja itajengwa
kwa Sh. milioni 200, kununua
madawati 857,000 kwa makaditio ya
kila dawati kununuliwa kwa Sh.
140,000 na pia kuchimba visima virefu
vya maji 4,800 ikiwa kila kisima
kitagharimu Sh. milioni 50.
Aidha, inaelezwa vilevile kuwa fedha
hizo (Sh. bilioni 120) zingeweza pia
kusaidia ujenzi wa maabara kwa shule
za sekondari na pia kuwapa mikopo
wanafunzi 80,000 kwa mwaka wa vyuo
vya elimu ya juu ikiwa kila mmoja
wao angepatiwa Sh. milioni 1.5.
Kiasi hicho cha fedha zinazoteketea
kwa mchakato wa katiba kingeweza
pia kuboresha miundombinu ya reli,
dawa za binadamu na mifugo na hata
shughuli ya usambazaji wa umeme
vijijini.
UREFU WA DAR HADI BUKOBA
Katika hatua nyingine, imefahamika
kuwa noti milioni 12 za Sh. 10,000
zinahitajika kukamilisha kiasi cha Sh.
bilioni 120 na noti hizo zinaweza
kupangwa kwa urefu katika barabara
itokayo jijini Dar es Salaam hadi
Bukoba yenye urefu unaokadiriwa
kuwa kilomita 1,379 na bado kiasi
kingine kitabaki.
Hesabu hizo zinatokana na ukweli
kuwa kwa uchunguzi wa NIPASHE,
urefu wa noti moja ya sh. 10,000 ni
sawa na sentimita 14.1, hivyo kwa
noti milioni 12, umbali wake kwa
kuzitandaza ni sawa na sentimita
169,200,000 au kilomita 1692 (kilomita
moja ni sawa na sentimita 100,000).
Kiasi hicho cha fedha zinazoteketea
kwa mchakato wa katiba kingeweza
pia kuboresha miundombinu ya reli,
dawa za binadamu na mifugo na hata
shughuli ya usambazaji wa umeme
vijijini.
WASOMI WAZUNGUMZA
Mhadhiri mwandamizi katika Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Dk.
Semboja Haji, alisema kilichotokea
kwenye mchakato wa katiba ni jambo
lililotegemewa.
Alisema mfumo wa watu walioteuliwa
kuunda Bunge Maalum la Katiba
ulidhihirisha kwamba hakuna
ambacho kingefanyika zaidi ya
kuligharimu taifa.
"Labda niseme tu kwamba siyo hali
ambayo sikuitegemea, kwa sababu
watu walioteuliwa kwenda kujadili
rasimu ya tume hawakuwa na uwezo
wa kutuletea kitu cha maana,"
alisema.
Dk. Semboja alisema pamoja na hali
hiyo kudhihirika mapema, anashangaa
kwa nini Usalama wa Taifa haukubaini
na kumshauri rais jambo la kufanya ili
kuepusha hasara na aibu ambayo
Taifa imepata kutokana na kuendelea
kwa vikao vya Bunge Maalum la
Katiba.
Alionya kuwa kama mfumo wa
kutumia wanasiasa utaendelea
kutumika mwaka 2016, itatuchukua
muda mrefu kupata Katiba mpya.
Ikiwa makubaliano ya sasa yatataka
mchakato huo uendelee mwaka 2016
baada ya uchaguzi wa mwakani,
italazimika kutungwa kwa sheria
itakayomtaka rais ajaye atekeleze
mchakato huo vinginevyo anaweza
kupuuzia.

No comments:

Post a Comment