Monday, September 22, 2014

TAKWIMU ZA MAUAJI YA ALBINO ZI

Shirikisho la Vyama vya Watu wenye
Ulemavu Tanzania (Shivyawata),
limeitaka serikali kupitisha adhabu
ya kunyongwa kwa wale wanaohusika
na mauaji ya Albino.
Akizungumza katika maadhimisho ya
Siku ya Amani Kimataifa ya Albino
jana jijini Dar es Salaam, Rais wa
Chama cha Albino Tanzania (Tas),
Joseph Tona, alisema kauli hiyo
imetokana na ongezeko la idadi ya
mauaji dhidi yao.
Kadhalika, takwimu za kutoka mwaka
2006 zinaonyesha kuwa Albino 74
wameshauawa kikatili, huku 56
wakinusurika kifo, na kati yao 11
wameongezewa ulemavu mwingine
wa kudumu.
“Tunaadhimisha siku ya amani
Tanzania, lakini hatuna amani kabisa,
wenzenu tunakatwa viungo na
kuuawa kama kuku bila huruma,
kingine cha ajabu makaburi 18 ya
albino wenzetu yamefukuliwa na miili
yao imetolewa, picha hii inaashiria
nini?” alihoji Tona.
Alisema hofu hiyo imesababisha
maziko yao kutokuwa na heshima
kama wengine kutokana na baadhi ya
familia kuwazika wapendwa wao kwa
siri na wengine ndani ya nyumba, au
kuweka zege nzito katika makaburi
kuzuia ufukuaji wa miili yao.
Alisema licha ya serikali kuweka
vikosi kazi katika kudhibiti mauaji
hayo, bado haisaidii kitu kutokana na
baadhi ya polisi na maofisa kuwa
miongoni mwa vinara wa kupokea
rushwa.
Kwa mujibu wa Tona, matukio zaidi
ya 120 ni kesi za mauji ya albino, kati
yake 11 ndiyo yaliyofikishwa
Mahakama, ambapo kati ya hizo kesi
tano tu zimeweza kutolewa hukumu
hadi sasa.
Akitoa ushuhuda mmoja kati ya
waathirika ambaye mikono yake
miwili imekatwa, Mariam Stanford,
mkazi wa Ngara, mkoani Kagera,
aliwataka wauaji wa albino
wanyongwe hadharani ili iwe
fundisho kwa wengine wenye tabia
kama hizo.
“Japokuwa Tanzania inasifika ndani
na nje kama kisiwa cha amani, tafsiri
hiyo ni kinyume kwani ni miongoni
mwa nchi zinazoongoza kwa mauaji
ya kikatili, hivyo mwito wangu kwa
viongozi wa dini tumieni midomo
yenu kupinga hali hii kwa sababu na
sisi tumeumbwa na Mungu na
tunastahili kuisha kama wengine,”
alisema Miriam.
Mkurugenzi wa Shirika la Under The
Same Sun, Vicky Ntetema, aliishauri
serikali kupitia vikosi kazi
vilivyochukua jukumu la kuchunguza
mauaji na ukatwaji wa viungo kwa
albino, kutangaza matokeo kwa umma
ili wahusika wachukuliwe hatua za
kisheria.
Pia, iuelezee umma matokeo ya kura
za siri zilizopigwa katika mikoa
tangu mwaka 2009 hadi sasa
zibainishwe wazi kwani nyingi
zimeonyesha waganga wa jadi
kutumiwa na na viongozi wa kubwa
katika kuwania nyadhfa mbalimbali
serikalini.
Kutokana na hofu hiyo, ameitaka
serikali kurejea mkakati wa mwaka
2009 uliotolewa na Waziri Mkuu
Mizengo Pinda, ili kupiga marufuku
leseni za waganga wa kienyeji na
wale wa jadi.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Dk. Seif Rashid, alizitaka taasisi
zilizopewa jukumu la kusimamia
vitendo hivyo vya kikatili dhidi ya
walemavu hususani albino kutekeleza
majukumu waliyopewa kisheria kwa
uadilifu mkubwa jamii ya Watanzania
ione haki inatendeka ili kudumisha
amani ya nchi.

  BOFYA HAPA KUUNGANA NASI INSTAGRAM

No comments:

Post a Comment