Wednesday, September 24, 2014

KATIBA MPYA YATAKA RAIS KUA NA MADARAKA ZAIDI

Rasimu ya Katiba inayopendekezwa
na Bunge Maalum la Katiba,
imeongeza madaraka ya Rais
maradufu na kuondoa matakwa ya
rais kuzingatia masharti ya
uthibitisho wa Bunge katika nafasi za
madaraka na kumuachia uteuzi wa
moja kwa moja.
Akiwasilisha rasimu hiyo bungeni
jana, Mwenyekiti wa Kamati ya
Uandishi, Andrew Chenge, aliyataja
mambo mbalimbali yaliyofutwa,
yaliyoongezwa na yaliyoboreshwa
katika Rasimu ya Jaji Warioba.
Kwa mujibu wa Rasimu iliyotolewa
Desemba 31, 2013 na Mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Mstaafu Joseph Warioba, ilipendekeza
nafasi zote za uteuzi kupendekezwa
na mabaraza ya kisekta kabla ya Rais
kufanya uteuzi miongoni mwa majina
hayo kisha kuthibitishwa na Bunge
Ibara ya 73 (3) ya Rasimu ya Warioba
imependekeza kuwa Katika
utekelezaji wa madaraka kama
ilivyoainishwa katika ibara ndogo ya
(1) na (2), Rais atazingatia masharti
kuhusu uthibitisho wa Bunge katika
nafasi za madaraka na vile vile
ushauri wa mamlaka za Serikali,
Bunge au Mahakama zilizopewa
madaraka ya kumshauri katika
kufanya uteuzi, kuanzisha au kufuta
nafasi za madaraka katika utumishi
wa Serikali.
Aidha, ibara ya 74 (1) ya Rasimu ya
Warioba ilipendekeza kuwa mbali na
kuzingatia masharti yaliyomo katika
Katiba hii, na sheria za nchi, Rais
atakuwa na wajibu wa kufuata na
kuzingatia ushauri atakaopewa na
mamlaka za nchi, na endapo
hakubaliani na ushauri aliopewa,
sharti atoe sababu katika Baraza la
Mawaziri kuhusu sababu ya
kutokubaliana na ushauri aliopewa.
Nafasi pekee ya uongozi ambayo
baada ya uteuzi wa Rais itapaswa
kuthibitishwa na Bunge ni ya Waziri
Mkuu, wakati Rasimu ya Pili ya Jaji
Warioba mbali na Waziri Mkuu,
ilipendekeza, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali, Jaji Mkuu, na
Mkurugenzi na Mashtaka
kuthibitishwa na Bunge.
Nafasi za uteuzi ambazo
hazitathibitishwa na Bunge ni
Mawaziri, Manaibu Waziri, Katibu wa
Bunge, Mwanasheria Mkuu,
Mkurugenzi wa Mashtaka, Katibu
Mkuu Kiongozi, Wakuu wa mikoa wa
Bara.
MAHAKAMA
Rasimu hiyo imependekeza Jaji
Mkuu, Naibu Jaji Mkuu, Jaji wa
Mahakama ya Juu, Naibu Jaji Mkuu,
Mwenyekiti wa Mahakama ya Rufani,
Makamu Mwenyekiti, ambao
watateuliwa na Rais kutoka majina
matatu yaliyopendekezwa na Tume ya
Utumishi wa Mahakama.
Wengine ni Msajili Mkuu wa
Mahakama atateuliwa kutokana na
mapendekezo ya Tume ya Utumishi
wa Mahakama, Mtendaji Mkuu wa
Mahakama atateuliwa kutoka majina
matatu ya watumishi wa umma
yaliyopendekezwa na Tume.
TUME YA HURU YA UCHAGUZI
Rasimu hiyo imependekeza
Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na
wajumbe wengine saba
watakaoteuliwa na rais baada ya
kupendekezwa na kamati ya uteuzi.
Aidha, Mkurugenzi wa Tume Huru ya
Uchaguzi atateuliwa na Rais baada ya
kupendekezwa na Tume ya Utumishi
wa umma.
MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA
Rasimu hiyo imependekeza Msajili wa
Vyama vya Siasa na Naibu Msajili,
watateuliwa na rais kutoka majina
matatu yaliyopendekezwa na Tume ya
Utumishi wa Umma.
TUME YA MAADILI YA VIONGOZI WA
UMMA
Imependekeza Mwenyekiti, Makamu
na wajumbe wa Tume ya Maadili ya
Viongozi wa Umma, wateuliwe na rais
kutoka majina yaliyopendekezwa na
Tume ya uteuzi
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA
UTAWALA BORA
Rasimu hiyo imependekeza
Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti
watateuliwa na Rais kutoka majina
yaliyopendekezwa na Tume ya uteuzi.
CAG
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG), atateuliwa na Rais
kutoka majina matatu
yaliyopendekezwa na Tume ya
Utumishi wa Umma.
VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Mkuu wa
Jeshi la Polisi (IGP), Mkurugenzi
Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa,
watateuliwa na Rais.
RASIMU YA JAJI WARIOBA
ILIPENDEKEZAJE?
Rasimu ya Jaji Warioba ilipendekeza
Mawaziri, Naibu Mawaziri,
Mwanasheria Mkuu, Katibu Mkuu
Kiongozi na Makatibu Wakuu, Jaji
Mkuu, Naibu Jaji Mkuu, Mwenyekiti,
Makamu Mwenyekiti na wajumbe saba
wa Tume Huru ya Uchaguzi,
Mkurugenzi wa Tume Huru ya
Uchaguzi, Msajili wa Vyama vya
Siasa, Mwenyekiti na Makamu
Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya
Viongozi na Uwajibikaji.
Wengine ni Mwenyekiti na Makamu
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za
Binadamu, CAG.Ambao watateuliwa
na Rais na kutothibitishwa na Bunge
bali kushauriana na Baraza la Ulinzi
na Usalama la Taifa ni Mkuu wa
Majeshi ya Ulinzi, Inspekta Jenerali
wa Polisi (IGP) na Mkurugenzi wa
Idara ya Usalama wa Taifa.
IBARA ZILIZOFUTWA
Kamati ya Uandishi BMK imewasilisha
bungeni Rasimu ya Katiba
inayopendekezwa ambayo imefuta
Ibara 28 zilizokuwemo kwenye
Rasimu ya Pili iliyoandaliwa na Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, huku
ikizifanyia marekebisho Ibara 186 na
kuingiza Ibara mpya 41.
Chenge alisema kufutwa kwa ibara
hizo pamoja na marekebisho
yaliyofanyika kwenye ibara nyingine
kunatokana na michango ya idadi
kubwa ya wabunge wa BMK wakati
wa mijadala ya kwenye kamati na
ndani ya Bunge na kutokana na
sababu maalum kuna maeneo ambayo
maoni ya wachache yamezingatiwa.
“Rasimu hii inazo Ibara 274, kati yake
ibara 233 zinatokana na rasimu
iliyowasilishwa kwenye bunge hili na
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ibara
186 zimefanyiwa marekebisho ya
kiuandishi na kimaudhui, ibara 47
hazijafanyiwa marekebisho yoyote,
lakini pia ibara 28 zimefutwa na
tumeingiza ibara mpya 41,” alisema
Chenge.
Rasimu ya pili ya Tume ya Mabadiliko
ya Katiba iliyowasilishwa bungeni na
aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo,
Jaji Joseph Warioba ilikuwa na sura
17 zenye ibara 271.
Katika Rasimu iliyowasilishwa jana
bungeni na Chenge kuna sura 19
zenye ibara 274, hivyo kuwepo kwa
ongezeko la sura mbili na ibara tatu
ikilinganishwa na Rasimu ya Jaji
Warioba.
MAMBO MAPYA
Kwa Mujibu wa Chenge miongoni
mwa mambo makubwa yaliyoongezwa
katika Sura ya Kwanza, Ibara ya Sita
inayozungumzia misingi ya utawala
bora jambo ambalo halikuwemo
kwenye Rasimu ya Jaji Warioba.
Katika Sura ya Pili kwenye Ibara ya 16
yamewekwa masuala yanayohusu
utafiti na maendeleo na katika ibara
ya 17 kuna Dira ya Maendeleo na
Ibara ya 18 inazungumzia Tume ya
Mipango ya Jamhuri ya Muungano na
matumizi ya masharti ya sura ya pili
yakiwa katika ibara ya 20.
Sura ya Tatu ibara ya 22 inayohusu
ardhi huku matumizi bora ya ardhi
yakizaa ibara ya 23 huku mwanamke
akipewa haki ya kumiliki na kutumia
ardhi kama ilivyokuwa kwa
mwanaume.
Aidha katika sura ya nne,
imeongezwa ibara inayozungumzia
utaratibu wa utwaaji wa mali ya umma
iliyotwaliwa na kiongozi aliyefanya
ubadhirifu.
MAMBO YALIYOFUTWA
Chenge aliyataja mambo ambayo
yamefutwa kutoka kwenye Rasimu ya
Jaji Warioba kuwa ni Muundo wa
Muungano wa Serikali tatu uliokuwa
katika Sura ya sita ambao
umebadilishwa na kuependekezwa
kuendelea na Muundo wa Serikali
mbili na nchi moja.
Mambo mengine ni ukomo wa
ubunge, wananchi kupewa mamlaka
ya kumwajibisha mbunge na Mawaziri
kutokuwa wabunge.
Kwa mujibu wa Rasimu
inayopendekezwa, nafasi ya ubunge
haitakuwa na ukomo wa kugombea,
wananchi watamwajibisha mbunge
kupitia uchaguzi baada ya mbunge
kumaliza kipindi chake cha uongozi
cha miaka mitano na mawaziri
wataendelea kupatikana miongoni
mwa wabunge.
YALIYOFANYIWA MAREKEBISHO
Baadhi ya mambo ambayo
yamefanyiwa marekebisho
ikilinganishwa na yalivyokuwa katika
Rasimu ya Jaji Warioba ni Tunu za
Taifa ambazo zimepunguzwa kutoka
saba na kubakia nne.
Tunu zilizowekwa kwenye Rasimu
mpya ni Lugha ya Kiswahili,
Muungano, utu na undugu pamoja na
amani na utulivu.
Katika Rasimu ya Jaji Warioba Tunu
zilizopendekezwa zilikuwa ni utu,
uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi,
uwajibikaji na lugha ya taifa.
Chenge alisema marekebisho mengine
yaliyoingizwa katika Rasimu ya
Katiba ni kuongezeka kwa haki za
wanawake, vijana, watoto, watu
wenye ulemavu, wazee na haki za
wasanii.
Marekebisho mengine yapo kwenye
sura ya sita inayohusu uraia, ambapo
watanzania wenye uraia wa nchi
nyingine hawatakuwa na uraia wa
nchi mbili, isipokuwa watapewa
hadhi maalum ya watu wenye asili au
nasaba ya Tanzania, tofauti na
mapendekezo ya Rasimu ya Jaji
Warioba iliyopendekeza watu wa aina
hiyo watakapokuwa ndani Jamhuri ya
Muungano watakuwa na hadhi kama
itakavyoainishwa katika sheria za
nchi.
Katika sura ya nane ya Rasimu
inayopendekezwa na BMK, Rais wa
Zanzibar atakuwa makamu wa pili wa
Rais na Waziri Mkuu atakuwa Makamu
wa tatu wa Rais huku ikitamka
kwamba makamu wa kwanza wa Rais
ni Mgombea Mwenza wa Rais wakati
wa uchaguzi.
Aidha katika sura hiyo ya nane,
Rasimu imependekeza idadi ya
mawaziri kuwa 30 na Naibu Mawaziri
kuteuliwa kutegemeana na mahitaji ya
Serikali.
Katika Rasimu ya Jaji Warioba
ambayo ililenga Muundo wa Serikali
tatu, ilipendekezwa idadi ya Mawaziri
wa Jamhuri ya Muungano na Naibu
Mawaziri haitazidi 15.
Marekebisho mengine yaliyofanywa
kwenye Rasimu inayopendekezwa na
BMK ni suala la Mgombea huru
ambalo katika rasimu hiyo
limewekewa masharti maalum, ikiwa
ni pamoja na idadi ya wapiga kura
wanaohitajika kumdhamini kwa ngazi
ya nafasi anayogomea, kipindi
ambacho amekoma kuwa
mwanachama wa chama chochote cha
siasa kabla ya siku ya uchaguzi,
kutojiunga na chama chochote cha
siasa katika kipindi ambacho atakuwa
kiongozi baada ya kuchaguliwa,
utaratibu wa kuainisha vyanzo vya
ndani na nje vya mapato vya
kugharimia kampeni za uchaguzi,
utaratibu wa kuainisha vigezo na sifa
zitakazotumiwa kuwapata viongozi
wa ngazi za juu kitaifa na kuweka
wazi ilani ya uchaguzi inayoonyesha
mipango ya uendeshaji wa nchi.
Katika Rasimu ya Jaji Warioba,
mgombea huru hakuwekewa mashariti
zaidi ya kuwa na sifa za ujumla
zinazomruhusu kugombea kwa
mujibu wa katiba.
Kwa mujibu wa Chenge, marekebisho
mengine ni idadi ya wabunge wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano
ambao wameongezeka kutoka 75
waliopendekezwa na Tume ya Jaji
Warioba hadi kufikia wabunge 360.
Katika Rasimu ya Pili ya Jaji Warioba
ilipendekezwa wabunge 70 wa
kuchaguliwa kupitia majimbo ya
uchaguzi, kati yao 50 kutoka
Tanganyika na 20 kutoka Zanziba,
huku pia ikipendekeza kuwepo kwa
wabunge watano wenye ulemavu
watakaoteuliwa na Rais.
Marekebisho mengine yaliyoingizwa
kwenye Rasimu inayopendekezwa na
BMK ni sifa ya mtu anayestahili
kugombea nafasi za kisiasa kama vile
udiwani, ubunge na urais.
Katika Rasimu ya Jaji Warioba
ilipendekezwa kuwa mtu mwenye sifa
ya kugombea nafasi ya Ubunge ni
lazima awe na elimu ya kidato cha
nne, lakini katika Rasimu
inayopendekezwa na BMK sifa hiyo
imeondolewa na badala yake mtu
anayegombea anapaswa kujua
kusoma na kuandika.
YALIYOFUTWA, KUBORESHWA
MUUNDO WA MUUNGANO
Ibara ya kwanza inayozungumzia
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Bunge Maalum la Katiba limefuta
mapendekezo ya rasimu ya iliyokuwa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa
kufuta Muungano wa serikali tatu na
badala yake imependekeza serikali
mbili kama ilivyo kwenye Katiba ya
mwaka 1977.
Katika Ibara 1 (i), Tume ya
Mabadiliko ya Katiba ilieleza kuwa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni
Shirikisho lenye mamlaka kamili
ambayo imetokana na Muungano wa
nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika
na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar
ambazo kabla ya makubaliano ya
Muungano ya mwaka 1964 zilikuwa
nchi huru.
Hata hivyo, Kamati ya Uandishi
imefuta neno 'Shirikisho' kwenye
ibara hiyo kwa maelezo kuwa
wajumbe wengi wamependekeza
Muungano wa serikali mbili.
Mapendekezo ya Kamati hiyo
yanasema kuwa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ni nchi yenye
mamlaka kamili ambayo imetokana na
Muungano wa nchi mbili za Jamhuri
ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar ambazo kabla ya Hati ya
Makubaliano ya Muungano ya tarehe
22 Aprili,1964 zilikuwa nchi huru.
Aidha, katika kifungu kidogo cha pili
cha Ibara hiyo, Tume ilipendekeza
kuwa Jamhuri ya Muungano ni
Shirikisho la kidemokrasia linalofuata
mfumo wa vyama vingi vya siasa,
usawa wa binadamu, kujitegemea,
utawala wa sheria na kuheshimu haki
za binadamu; hata hivyo, kamati ya
uandishi imefuta neno 'kujitegemea'
kwa madai kuwa linaleta kasoro ya
mtiririko.
“Kwa msingi huo, Kamati ya Uandishi
imeiandika upya Ibara hii kama
inavyosomeka kwenye Ibara ya 1 ya
Rasimu hii ya Katiba
inayopendekezwa. Neno hilo
(shirikisho), lilifutwa kwa kuwa
mapendekezo yaliyotolewa na
Wajumbe walio wengi ndani ya
Kamati zote kumi na mbili za Bunge
Maalum yalilenga kuwepo kwa
Muundo wa Serikali Mbili," alisema
Chenge.
Kadhalika, Kamati ya Uandishi
imeongeza ibara ndogo mpya ya (3)
kwa kutoa mamlaka kwa Bunge
kutunga sheria itakayoainisha na
kufafanua mipaka ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Kamati hiyo pia imeongeza sikukuu
za taifa kwa kuongeza maadhimisho
ya kitaifa katika Ibara ya tatu ya
rasimu.
“Katika Ibara hii, Kamati sita kati ya
Kamati Kumi na mbili zilipendekeza
kufanya marekebisho kwenye Ibara ya
(3)(1) kwa kuongeza aya mpya ya (d)
kwa ajili ya kuongeza maneno na
maadhimisho ili mbali na Sikukuu za
Taifa zilizoainishwa katika Ibara hii,
kuwapo pia na maadhimisho mengine
ya kitaifa."
Bunge Maalum pia limefuta Ibara ya
tano ya rasimu ya Katiba iliyokuwa
inazungumzia Tunu za Taifa kwa
madai kuwa mambo yaliyotajwa kuwa
Tunu ni msingi wa utawala bora.
Katika Ibara hiyo, Tume ilipendekeza
kuwa Jamhuri ya Muungano itaenzi
Tunu saba ambazo ni (a) utu, (b)
uzalendo (c) uadilifu, (d) umoja, (e)
uwazi, (f) uwajibikaji na (g) lugha ya
Taifa.
Badala yake, Kamati ya Uandishi
imesema: “Kuwa Tunu na misingi ya
utawala bora ni mambo mawili tofauti,
Kamati inapendekeza kuifuta Ibara ya
5 na kuiandika upya.”
Baada ya kufuta, Kamati hiyo
imependekeza Tunu ziwe ni (a) amani
na utulivu, (b) haki na usawa wa
binadamu, (c) usawa wa jinsia na (d)
Lugha ya Kiswahili.
Kamati imeongeza Ibara ya 6
inayoeleza misingi ya utawala bora
ambayo ni (a) uadilifu; (b)
demokrasia; (c) uwajibikaji;(d)
utawala wa sheria; (e) ushirikishwaji
wa wananchi; (f) haki za binadamu;
(g) usawa wa jinsia; (h) umoja wa
kitaifa; (i) uwazi; na (j) uzalendo.
Hata hivyo, Chenge alisema baadhi
ya Ibara za Rasimu za Katiba zimebaki
kama zilivyo kwa kuwa maudhui yake
yanajitosheleza na nyingine
zimefutwa kwa kuwa maudhui yake
yamezingatiwa katika Ibara nyingine.
Sababu nyingine ya kufuta ni kwa
kuwa maudhui yake yamebebwa
katika mapendekezo mengine;
maudhui yake yanapaswa kuzingatiwa
katika sheria za nchi; maudhui ya
Ibara nyingine yamehamishiwa
kwenye Ibara nyingine ili kuweka
pamoja maudhui yanayofanana; na
maudhui mengine yamegawanywa
katika Ibara ndogo tofauti kwa lengo
la kuyaweka wazi zaidi.
MAADILI NA MIIKO YA VIONGOZI WA
UMMA
Katika rasimu ya Tume, Ibara ya 14 (i)
(a), (b) na (c), pamoja na mambo
mengine, ilipendekeza kuwa kiongozi
wa umma atatakiwa kulinda hadhi ya
ofisi yake na kuhakikisha
hatosababisha mgongano wa maslahi
ya umma na binafsi; lakini Kamati ya
uandishi imefuta na kupendekeza
sharti hilo lijumuishwe kwenye
sheria.
Kamati hiyo inapendekeza kufuta na
kuiandika upya Ibara hiyo ili
kubainisha miiko ya msingi katika
uongozi wa umma na kuacha mambo
mengine ya kiutendaji yazingatiwe
katika Sheria itakayotungwa na
Bunge.
“Sababu ya mapendekezo haya ni
kuwa, maudhui ya Ibara hii ya Rasimu
ya Tume, yanaelezea mambo mengi
yakiutendaji na kiutawala ambayo ni
muhimu yakaainishwa katika Sheria
zitakazotungwa na Bunge ili
kurahisisha utekelezaji pindi
kunapotokea mabadiliko."
“Lengo la maboresho ni kuhamishia
masuala haya kwenye sheria za nchi
kutokana na ukweli kwamba
yanabadilika mara kwa mara kutokana
na wakati.”
Bunge Maalum pia limeongeza sura
mbili mpya ambazo hazikuwamo
katika rasimu ya Tume ambazo ni ile
inayohusu Ardhi, Maliasili na
Mazingira na Sura inayohusu Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar, Baraza la
Mapinduzi la Zanzibar na Baraza la
Wawakilishi la Zanzibar.
Aidha, Sura ya Pili ilikuwa na sehemu
moja sasa inapendekezwa kuwa na
sehemu tano na pia Ibara nyingine
mpya zimependekezwa katika Rasimu
ya Katiba inayopendekezwa.
Kamati hiyo imeeleza sababu za
kuridhia kuongeza sura hiyo ni
umuhimu wa ardhi, maliasili na
mazingira katika maendeleo ya nchi
kwa kuwa ni vitu vinavyogusa maisha
ya kila siku ya Watanzania wengi
wakiwamo wafugaji, wakulima,
wavuvi na wachimbaji wa madini.
Alisema lengo ni kuhakikisha raia wa
Tanzania pekee ndiyo wenye haki ya
kumiliki ardhi.
SIFA YA KUGOMBEA UBUNGE
Sifa ya elimu kwa mtu anayegombea
ubunge imependekezwa kuwa awe
anajua kusoma na kuandika Kiswahili
au Kiingereza.Pendekezo hilo linafuta
sharti la awali la kuwa na elimu ya
kidato cha nne, lililopendekezwa na
rasimu ya katiba iliyowasilishwa
katika Bunge Maalumu la Katiba na
aliyekuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba.
Pendekezo la kufuta sharti hilo
lililomo kwenye ibara ya 117 (1) (b)
lilitolewa na Kamati ya Uandishi ya
Bunge hilo kupitia Mwenyekiti wake,
Andrew Chenge, bungeni jana.
Chenge, ambaye ni Mbunge wa
Bariadi Magharibi, alisema pendekezo
hilo limetolewa na kamati yake ili
kutoa fursa kwa watu wenye uwezo
wa kugombea wafanye hivyo, ikiwa ni
pamoja na kuondoa dhana ya uwapo
wa nchi washirika na kulifuta neno
hilo kila linapojitokeza ili kuendana
na mfumo wa serikali mbili
unaopendekezwa kwa sasa.
Pia alisema kamati imeridhia
pendekezo la kuwapo mgombea huru
katika nafasi ya ubunge na kwamba,
pendekezo la kumzuia mtu mwenye
madaraka kugombea nafasi hiyo,
limezingatiwa na kamati kwa kufuta
sharti hilo, ili lizingatiwe katika ibara
nyingine.
Alisema kamati saba za Bunge hilo
zimependekeza aya ya (d) ya ibara
ndogo ya (1) ifutwe na kamati tano
zimependekeza Ibara hiyo ifanyiwe
marekebisho madogo, yakiwamo
kuongeza ibara ndogo ya (1) (g) ili
kutoa fursa kwa Rais kutengua uteuzi
wa mbunge wa kuteuliwa.
Chenge alisema kamati yake baada ya
kupitia mapendekezo hayo,
imeongeza aya mpya ya (h)
inayoweka sharti la mbunge
aliyetokana na mgombea huru
kupoteza sifa za kuwa mbunge
kutokana na kujiunga na chama
chochote cha siasa.
Kuhusu ibara ya 129 inayohusu haki
ya wapiga kura kumwajibisha
mbunge, alisema kamati moja
imependekeza Ibara hiyo ibaki kama
ilivyo kwenye rasimu ya tume, lakini
kamati saba zimependekeza ifutwe na
kamati nne zimependekeza
marekebisho madogo, ikiwamo
kuwapo kwa haki ya wapigakura
kumwajibisha mbunge, ambaye
ameshindwa kuwasilisha au kutetea
kero za wapigakura wake.
Alisema kamati yake baada ya
kutafakari maoni hayo, inapendekeza
ibara hiyo ifutwe kwa kuwa haki
inayopendekezwa inaweza kutumika
vibaya, ikiwamo kumwekea vikwazo
vya kiutendaji mbunge aliyeko
madarakani.
Pia wapigakura wanayo haki ya
kumwajibisha kwa kutompigia kura
mbunge katika kipindi cha miaka
mitano endapo wananchi wataona
mbunge anayewawakilisha hafai,
wanaweza kumwajibisha.
“Kwa kuzingatia mapendekezo hayo
Kamati ya Uandishi inapendekeza
Ibara hii ifutwe,” alisema Chenge.
IBARA YA 132 KUHUSU SPIKA
Chenge alisema kamati yake
imependekeza kuwa ibara hiyo ibaki
kama ilivyo kwenye rasimu ya tume
kwa kuwa maudhui yake
yanajitosheleza.
Hata hivyo, alisema baada ya
kuchambua na kuzingatia
mapendekezo ya kamati za Bunge na
mijadala bungeni, kamati yake
imeifuta na kuiandika upya ibara
ndogo ya (1) ili kumuwezesha Spika
wa Bunge kuchaguliwa kutoka
miongoni mwa wabunge au watu
wenye sifa za kuwa wabunge.
Pia alisema kamati yake imekubaliana
na pendekezo la kufuta neno
“Mbunge” katika ibara ndogo ya (2) ili
kumwondoa mbunge katika orodha ya
watu wanaokosa sifa za kugombea
nafasi ya Spika.
Imeandaliwa na Emmanuel Lengwa,
John Ngunge, Jacqueline Massano na
Editha Majura, Dodoma na Salome
Kitomari, Muhibu Said na Restuta
james (Dar).

No comments:

Post a Comment