Wednesday, September 24, 2014

SANAA ZA UTAMADUNI WA TANZANIA ZAENDELEA KUBADILIKA

Licha ya kuwapo mawimbi ya
utandawazi yanayoyumbisha sanaa za
ufundi za tamaduni mbalimbali dunia,
Tanzania imeendelea kuwa imara
kwani sanaa zenye utamaduni wake
zimeendelea kukubalika maeneo
mengi duniani.
Ndiyo maana michoro na vinyago vya
marehemu George Lilanga na Edward
Tinga Tinga vinaonyeshwa katika
mataifa mengi duniani.
Hata hivyo kazi za wasanii hao zina
thamani zaidi ng’ambo hasa Ulaya
kuliko nchini.
Profesa wa Sanaa kutoka Uingereza,
Augustus, Casely, alisema hayo juzi
kwenye semina iliyokutanisha
wataaluma wa magwiji wa sanaa
wakiwamo wanahistoria ya sanaa,
wasanii na wapenda kazi za kisanii
iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Semina hiyo ni sehemu ya kuenzi kazi
za msanii nguli hayati George Lilanga,
ambaye Nyumba ya Makumbusho ya
Taifa jijini Dar es Salaam, imeandaa
maonyesho ya kimataifa ya sanaa
zake.
Profesa Casely alisema kazi za
wasanii wa Tanzania zimekubalika
Ulaya ambako watu wana uga na
kumbi za kazi za Lilanga
wanazozitangaza kwenye miji
mbalimbali hasa Uingereza. Hayati
Lilanga kwa mujibu wa Mkurugenzi
Mkuu wa Makumbusho ya Taifa,
Profesa Audax Mabulla, alifanyakazi
nyingi za kisanii katika miaka 1970 na
1980, akichora, kuchonga na
kufinyanga vinyago maarufu vya
‘mashetani.’
“Lilanga alikuwa na kazi za kisanii
zilikuwa zinawafanya watu
wachemshe bongo, wafikirie na
kujifunza ili kuelewa zaidi. Ukiangalia
‘mashetani’ unalazimika kutumia
kichwa kutafsiri na kuujua ujumbe
uliopo,” alisema Profesa Mabulla.
Semina hiyo ambayo ilihudhuriwa na
Profesa gwiji wa historia ya sanaa
Elias Jengo wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, ilijadili mada kadhaa kuhusu
hali ya kazi za sanaa za ufundi za
kileo na zile za kitamaduni.
Akijibu swali la NIPASHE kwanini kazi
hizo ziwe na mapenzi zaidi na
wageni, Mhifadhi Mkuu wa
Makumbusho ya Taifa, Achiles Bufure,
alisema ni matokeo ya kutofuatilia na
kuhamasiha umma, lakini sasa
Makumbusho ina ari mpya ya
kuendeleza sekta hiyo.
Alitaja mikakati ya kuendeleza kazi za
sanaa kuwa ni kuwakusanya wasanii
pamoja na kazi zao ili kuwaendeleza
na kwamba hatua mojawapo
zilizochukuliwa ni kuwaandalia uga
maalumu ndani ya jumba hilo.
Aliwasifu wasanii kwa kuhifadhi
sanaa za asili za kudumisha
utamaduni na pia usanii wa kisasa
kwa ajili ya biashara na kupata
masoko sehemu mbalimbali kama
ilivyo kwa Lilanga

No comments:

Post a Comment